Wanachokosea Watengenezaji Wengi wa Website (Tovuti)
Hivi ulishawahi jiuliza ni kwanini una website nzuri na inavutia kimuonekano lakini haikuongezei mauzo, jambo linalopelekea kupoteza fedha nyingi za hosting na domain kila mwaka bila kupata faida uliyotarajia?
Usijali ndani ya dakika chache tu ntakupa siri ambayo wengi hawaijui, imekuwa bahati kwako kukutana na andiko hili.
Website ina vipengele vikuu tisa (Kuanzia header mpaka footer). Hivyo vipengele tutavijadili kwa kina katika maandiko yajayo lakini leo nitagusia hasa kipengele cha kwanza ambacho ni Header (Kichwa cha Tovuti), unajua kwa nini nimechagua kipengele hiko? Kwa sababu kama header yako itakuwa sawa basi utakuwa umemaliza 50% ya website yako yote.
Header ni ile sehemu ya juu kabisa katika webpage yako ambayo huwa ya kwanza kuonekana katika website, na hapo ndipo umuhimu wake unapoanzia, hapo ndipo mtembeleaji wako (visitor) anapofanya maamuzi aidha ya kuendelea kubaki katika website au ajiondokee zake tu.
Watafiti kutoka katika kampuni ya Microsoft wakiongozwa na ndugu Chao Liu wanasema ndani ya sekunde 10 za mwanzo punde tu baada ya mtembeleaji/mteja (visitor) kufika katika website yako ndipo maamuzi ya aidha aendelee kubaki au aondoke katika website hiyo yanapotokea.
Kwa mantiki hiyo basi kuna haja kubwa ya kutengeneza header itakayowavutia wateja wako ndani ya hizo sekunde 10 na kuamua kuendelea kubaki. Unaweza kuwa na maswali mengi sana hasa hiyo header itakayomvutia mteja iweje, basi kaa chini, vuta pumzi kisha piga glasi ya maji nakuelekeza sasa hivi.
Ukiwa unatengeneza header ya website basi jiulize maswali matatu yafuatayo:
- Unatoa huduma au bidhaa gani?
- Hiyo huduma/bidhaa vipi inatatua changamoto za mteja wako?
- Mteja afanye nini ili apate hiyo huduma/bidhaa yako?
Majibu ya maswali hayo matatu ndio yanaenda kutengeneza header itakayoshika ‘attention’ za watembeleaji wako. Wakati unaandika na kuelezea huduma unayotoa sambamba na vipi inatatua changamoto za walengwa wako basi hakikisha unatumia maneno machache, marahisi na yenye kueleweka (Usilete ufundi wa maneno hapo) ikiwezekana tumia formula ya K.I.S.S (Keep it Simple and Short). Chukulia mfano hapo chini jinsi mambo mawili nilivyoyatumia kutengeneza sehemu ya header yangu:
Mfano 1: Wakaribishe na wape furaha wageni wako, kwa kuwapa vitafunwa/snacks tamu.
Mfano 2: Tunatoa huduma ya kukupikia chakula muda wowote, hivyo utaokoa muda wako mwingi.
Mfano 3: Nguvu zako za kiume zitarudi na ndoa yako itaimarika, tumia virutubisho vyetu vilivyothibitishwa na wataalamu.
Tuendelee sasa, jambo la tatu muhimu katika header yako ni CTA (Call to Action) kwa tafsiri isiyorasmi ni nini afanye ili kupata hiyo huduma/bidhaa yako. Tukumbuke kuna aina kuu mbili za CTA ambazo ni Direct CTA, ambayo hiyo inamfanya mteja achukue hatua ya moja kwa moja mfano:
‘Nunua sasa’ (Buy now, Shop now)
‘Tupigie sasa’ (Call now) nk
Aina ya pili ni Transitional CTA hii hupitia hatua kadhaa kabla ya mteja kununua huduma/bidhaa yako mfano;
‘Jifunze zaidi’ (learn more)
‘About Us’ (kuhusu sisi) nk
Sasa katika header yako ya website ni vyema kutumia aidha Direct CTA au zote mbili lakini sio Transitional CTA peke yake.
Kutokana na tafiti zilizofanywa, watu wengi wakifungua website macho yao hutazama katika muundo wa herifu Z, yaani wanaanza kuangalia juu kushoto, kisha juu kulia, kisha chini kidogo katikati, kisha chini kushoto na kumalizia chini kulia, hivyo basi unashauriwa CTA button yako uiweke sehemu mbili ambapo ni kulia juu na katikati ya header baada ya maelezo ya awali.
Cha mwisho lakini sio kwa umuhimu ni tumia picha katika header yako ambayo inaendana unachokifanya ili kuongeza mvutio zaidi (unaweza iweka pembeni au ukaifanya kuwa background yako, tumia designing skills hapo)
Ukifanikiwa kufuata mambo haya matatu basi 50% ya website yako itakuwa imekamilika, kazi ni kumalizia 50% zilizobaki ambazo zinapatikana katika sehemu zengine za website isiyokuwa header.
Kama umeelewa vizuri basi tengeneza mifano ya header kwa kutumia kanuni tulizozisoma, kisha tuma katika comment section hapo chini.